Version: 2.1

Ubatizo

Hadithi

(Mathayo 3:11, 13-17; 28:18-20)

Muda mfupi kabla ya Yesu kuanza kufundisha na kuponya watu, alienda kwenye Mto Yordani ili abatizwe. Nabii aliyeitwa Yohana alikuwa pale akiwaita watu waache dhambi zao kwa sababu Mwokozi alikuwa anakuja upesi. Yesu alikuwa Mwokozi waliyekuwa wakimngojea!

Yesu hakuwa na dhambi ya kutubia, bali alitaka kubatizwa na Yohana ili awe mfano kwetu sisi kuufuata na kuonyesha kwamba alikubaliana na ujumbe wa Yohana. Mwanzoni Yohana hakutaka kumbatiza Yesu na akamwambia, “Mimi nahitaji kubatizwa na wewe!” Yohana alijua kwamba Yesu alikuwa mkuu sana kuliko yeye. Hata hivyo, baada ya Yesu kumwambia Yohana kwamba lilikuwa jambo linalofaa kufanya, Yohana alikubali kumbatiza.

Yohana alimbatiza Yesu. Kwa hiyo Yesu akashuka chini ya maji na alipopanda kutoka majini, sauti ya Mungu kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa; nimependezwa naye.”

Mwishoni mwa huduma yake duniani, Yesu aliamuru wafuasi wake waende na kuwafanya watu wa mataifa yote ya ulimwengu kuwa wanafunzi na kuwabatiza katika jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Pia walipaswa kuwafundisha kutii kila kitu ambacho Yesu aliwaamuru. Wanafunzi wake walifanya kama walivyoamuru, na kila mahali walipoenda, waliwabatiza wale walioamua kuwa wafuasi wa Yesu.

Jizoeze kusimulia hadithi tena!

Maswali

  1. Je, unajifunza nini kuhusu ubatizo kutokana na hadithi hii?
  2. Unapaswa kutii nini?

Maana ya ubatizo

Neno “ubatizo” linamaanisha “kuzamisha” kama utakaso au kuosha. Kama vile Yesu alivyobatizwa, kila mtu anayemwamini anahitaji kubatizwa pia.
Yesu anawaamuru wafuasi wake mwishoni mwa Injili ya Mathayo:
“... mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” (Mathayo 28:19)
Maana ya mstari huu inakuwa wazi katika Matendo ya Mitume 2:38 (mstari wa kumbukumbu):

Petro akajibu, “Ni lazima kila mmoja wenu atubu dhambi zake na kumgeukia Mungu, na kubatizwa kwa jina la Yesu Kristo mpate ondoleo la dhambi zenu. Kisha mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.”

Utakaso kwa jina la Baba...

Kuungama dhambi na toba

Tunaungama dhambi zetu na kuziacha. Hatufagii makosa yetu chini ya kapeti, lakini tunayataja na kukiri (1 Yohana 1:9). Tunazungumza mahali tulipoishi kinyume na mapenzi ya Mungu. Tunaomba msamaha kwa Mungu kisha tuache kufanya mambo haya. Kwa msaada wa Mungu tunabadili mawazo na tabia zetu na kuishi kupatana na mapenzi ya Mungu.

Utakaso kwa jina la Mwana...

Ubatizo wa maji katika jina la Yesu Kristo

Ubatizo wa maji pia unaitwa “kuoshwa kwa kuzaliwa upya” (Tito 3:5).
Warumi 6:1-11 inaeleza maana hii:
Vile vile Yesu alizikwa na kisha kufufuka tena, tunaingia chini ya maji katika ubatizo na kutoka ndani ya maji na maisha mapya. Asili yetu ya zamani ya dhambi inakufa na sisi si tena “watumwa wa dhambi”. Hiyo ina maana kwamba hatupaswi tena kutenda dhambi. Sasa sisi ni “kiumbe kipya” (2 Wakorintho 5:17). Katika ubatizo tunazika maisha yetu ya kale na maisha mapya yanaanza, maisha mapya kabisa yanayoongozwa na mfano wa Yesu.

Utakaso kwa jina la Roho Mtakatifu...

Kupokea Roho wa Mungu

Mungu anataka kutupa Roho wake. Roho Mtakatifu ni kama “nguvu za Mungu” kwetu: Anatusaidia kufanya mapenzi ya Mungu na kumpinga shetani. Anasababisha matunda mema kama upendo, furaha, amani na uvumilivu kukua ndani yetu (Wagalatia 5:22).
Tunapopokea Roho wa Mungu, kitu hufanyika ndani yetu na hii inakuwa dhahiri kwa nje pia (mfano: Matendo ya Mitume 19:6). Tunapokea karama za Roho (1 Wakorintho 12:1-11 na 14:1-25). Hizi ni tegemezo kwetu na tunazitumia ili wengine wapate uzoefu wa nguvu za Mungu pia na sisi tuweze kuwafanya wanafunzi.

Kujitayarisha kwa ubatizo wako

Unaweza kusherehekea imani yako wakati wa ubatizo wako!

  • Ubatizo unapaswa kuwa wakati gani?
  • Tunapaswa kualika nani?
  • Wakati wa ubatizo wako unaweza kuandaa hadithi yako na Mungu kumwambia kila mtu jinsi Mungu alikuokoa na kukubadilisha.

Tenga wakati wa kubatizwa haraka iwezekanavyo. Pitia maswali ya ubatizo na utatue maswali yoyote.

Maswali ya ubatizo

  1. Je, uliungama dhambi zako kwa Mungu?
  2. Je, unajua na kuamini kwamba Mungu amekusamehe dhambi zako zote kupitia dhabihu ya Yesu?
  3. Je, uko tayari kuyazika maisha yako ya zamani na kuanza maisha mapya na Mungu?
  4. Je, umejitolea kumfuata Yesu na kutorudi nyuma?
  5. Je, utaendelea kumfuata Yesu hata wakikudhihaki, kukupiga, familia yako ikikufukuza, au utapata matatizo mengine?
  6. Je! Unataka kumpokea Roho Mtakatifu?